Friday, December 28, 2012

MAMENEJA VITANI! Wenger, Pardew wataka adhabu kwa Fergie!!

>>FA YAWAANDIKIA BARUA REDKNAPP & MANCINI KUJIELEZA!!
>>FERGIE AMPANDISHIA PARDEW!!
WENGER_AHIMIZA12
WAKATI FA, Chama cha Soka England, kimethibitisha kuwaandikia Barua za kuwataka kujieleza, Mameneja wa Man City na QPR, Roberto Mancini na Harry Redknapp, kufuatia kauli zao baada ya Mechi zao za kulalamika kuhusu Marefa na kudokeza uchezeshaji usio wa haki, Mameneja wa Arsenal, Arsene Wenger, na wa Newcastle, Alan Pardew, wamesema Sir Alex Ferguson alistahili Kadi Nyekundu kwa kubishana na Marefa kwenye Mechi kati ya Manchester United na Newcastle iliyochezwa Boxing Dei.

Akijiingiza kwenye mzozo huo, Arsene Wenger amesema Sir Alex Ferguson alipaswa kuadhibiwa na Refa Mike Dean kwa kitendo chake cha kabla Kipindi cha Pili kuanza kwenye Mechi kati ya Manchester United na Newcastle cha kumvaa Refa Mike Dean na kumlalamikia kisha kumkabili Refa wa Akiba Neil Swarbrick na pia Refa Msaidizi Jake Collin.

Katika Mechi hiyo ambayo Man United walishinda Bao 4-3, Ferguson alikuwa amekasirishwa na Refa Mike Dean kufuta Ofsaidi iliyotolewa ishara na Msaidizi wake Jake Collin na kuamua ni Bao kwa vile Jonny Evans alijifunga mwenyewe.

Wakati Kipindi cha Pili kinataka kuanza, Ferguson alimvaa Refa Mike Dean na kumlalamikia kisha akamvaa Refa wa Akiba Neil Swarbrick na pia Refa Msaidizi Jake Collin.

Lakini FA ilithibitisha jana kuwa Sir Alex Ferguson hatachukuliwa hatua yeyote kwa vile Refa Mike Dean hakutaja lolote kwenye Ripoti yake ya Mechi.

Wenger amesema Sheria ni msumeno na Refa Mike Dean alipaswa kumwadhibu Ferguson.

Arsene Wenger ashawahi kukumbana na Kadi Nyekundu toka kwa Refa Mike Dean Agosti 2009 alipotolewa Uwanjani kwa kuipiga teke chupa ya maji wakati Arsenal inachapwa 2-1 na Man United Uwanjani Old Trafford.

WAKATI HUO HUO, Sir Alex Ferguson amemshambulia Meneja wa Newcastle, Alan Pardew kwa kutamka kuwa alipaswa kupewa Kadi Nyekundu kwa kubishana na Refa Mike Dean na Wasaidizi wake wakati Newcastle ilipochapwa 4-3 na Man United Uwanjani Old Trafford.

Ferguson amejibu mapigo kwa kusema: “Alan Pardew amejitokeza na kuniponda mimi. Yeye ndio mbaya zaidi kwa kuvamia Marefa, anadiriki hata kuwasukuma na kisha analeta mzaha kuhusu hilo! Ameshasahau msaada niliompa!”

Ferguson ameongeza: “Sikufanya kosa! Sikutoa kashfa yeyote! Nlikuwa nikiongea na Refa tu! Tatizo ni kuwa tupo Klabu kubwa na mimi ni Meneja wa Klabu kubwa Duniani hivyo kila kitu kinakuzwa! Sio Newcastle Klabu ndogo iliyo huko Kaskazini Mashariki!”

Pardew aliwahi kufungiwa Mechi mbili na kudundwa Faini ya £20,000 kwa kumsukuma Refa Msaidizi wakati Newcastle inaifunga 2-1 Tottenham Hotspur hapo Tarehe 18 Agosti.

HIVI PUNDE TU, FA, Chama cha Soka England, kimethibitisha kuwaandikia Barua za kuwataka kujieleza, Mameneja wa Man City na QPR, Roberto Mancini na Harry Redknapp, kufuatia kauli zao baada ya Mechi zao za kulalamika kuhusu Marefa na kudokeza uchezeshaji usio wa haki, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni za FA.

Mancini, Meneja wa Man City, alilalamika kuhusu Refa Kevin Friend baada kufungwa 1-0 na Sunderland kwenye Mechi ya Ligi Kuu England iliyochezwa Desemba 26 kwa Refa huyo kutopiga Filimbi ya Faulo aliyochezewa Mchezaj wake Pablo Zabaleta na badala yake kuachia mpira uchezwe na kuzaa Goli la Adam Johnson, Winga wa zamani wa Man City, lililowaua City 1-0.

Mancini alidai: “Pengine Refa alivimbiwa na Mlo wa Krismasi! Haiwezekani Waamuzi wawili wasione tukio hilo! [Akimaanisha Refa Na Msaidizi wake]”

Nae Harry Redknapp, Bosi wa QPR, yuko matatani baada ya kuhamaki na maamuzi ya Refa Chris Foy ambayo alidai ni ‘Skandali!’ wakati walipofungwa 2-1 na West Brom na kutupwa mkiani mwa Ligi Kuu England Siku ya Boxing Dei.

Refa Chris Foy alilikubali Goli la kujifunga mwenyewe Kipa Robert Green ambae alionekana akibanwa waziwazi na Mchezaji wa WBA, Marc-Antoine Fortune, na pia aliwayima Penati ya wazi mwishoni baada ya Beki Liam Ridgewell kuunawa mpira.

Redknapp amewaka: "Ile ni Faulo ya wazi kwa Kipa wetu na ile ni Penati ya wazi! Hii ni kashfa!”

Msimamo wa FA kwa Mameneja ni kwamba hawatakiwi kuwalaumu Marefa kuhusu maamuzi yao na wakifanya hivyo wanaandikiwa Barua kutaka maelezo yao na kama hayaridhishi hufunguliwa Mashitaka.

1 comment: