PATA HABARI KAMILI:
Release No. 094
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Juni 2, 2013
TAIFA STARS, SUDAN ZATOKA SULUHU
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)
imetoka sare ya bila kufungana na Sudan (Nile Crodcodile) katika mechi
ya kujipima nguvu iliyochezwa leo (Juni 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi
Bamlak Tessema wa Ethiopia ilikuwa sehemu ya maandalizi kwa timu zote
ambazo wikiendi ijayo zinacheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Wakati Stars itakuwa ugenini nchini Morocco, Sudan itacheza nyumbani
dhidi ya Ghana.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager ilicheza vizuri mechi hiyo, hasa kipindi cha pili ambapo
ilifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini ama
washambuliaji walipiga nje au mipira yao kuokolewa na kipa Ehab
Abdelfatahh wa Sudan.
Washambualiji wa Stars akina Khamis
Mcha, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba wakiongozwa na John Bocco walilitia
msukosuko mara kwa mara lango la Sudan ambalo lilikuwa chini ya beki wa
kati Nadir Eltayeb ambaye alifanya kazi ya ziada dakika ya 72 kuokoa
mpira uliokuwa ukielekea wavuni.
Stars katika mechi hiyo iliwakilishwa na
Juma Kaseja, Nadir Haroub/Vicent Barnabas, Shomari Kapombe, Kelvin
Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John
Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba/Khamis Mcha na Simon Msuva/Athuman
Idd.
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia,
Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka
timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani
nchini Brazil.
Timu inaondoka kesho alfajiri kwenda Morocco kwa kupitia Cairo, Misri ambapo inatarajia kuwasili Casablanca saa 8 mchana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Addis Ababa
No comments:
Post a Comment