Friday, May 31, 2013

MAN UNITED: NANI KUIMARISHA KIUNGO?

FABREGAS, ALCANTARA AU STROOTMAN??
 CESC_FABREGAS
KEVIN_STROOTMAN
INAAMINIKA, kitu cha kwanza kabisa kwa Meneja mpya wa Manchester United, David Moyes, ni kuimarisha Idara ya Kiungo ya Timu hiyo ambayo Miaka nenda rudi ndio dhaifu kupita nyingine na udhaifu huo unazidi baada ya kustaafu kwa Paul Scholes, kufifia kwa Anderson, kutotabirika kwa Tom Cleverley na umri kuyoyoma kwa Michael Carrick lakini ‘wakombozi’ wanatajwa kuwa ni Cesc Fabregas na Thiago Alcantara wa Barcelona na Kevin Strootman wa PSV.

NANI WANAFAA NA NANI WATAPATIKANA?
Habari za ndani ya Barcelona zinasema kuwa wao wako tayari kumuuza Cesc Fabregas ikiwa Klabu itafikia Dau la Pauni Milioni 25 kiwango ambacho Man United wako tayari kulipa lakini inaelekea Dau hilo linaweza kupanda baada ya Man City kutia mkono na wao kuonyesha nia ya kumnunua Kiungo huyo mwenye akili ya mpira ambae alikuwa Nahodha wa Arsenal.
Thiago_Alcantara
Hata hivyo, Klabu hizo za Jijini Manchester zinaweza tu kumnasa Fabregas, mwenye Miaka 26, ikiwa tu Arsenal itatamka kuwa haitaki kumnunua kwa vile Mkataba wake wa kumuuza kwa Barcelona una kipengele kuwa hawezi kuuzwa Klabu nyingine hadi Arsenal ithibitishe haitaki kumnunua.

Zipo dalili Arsenal haitaki kumrudisha Fabregas na kilichobaki ni Klabu ipi ya Manchester itamnasa ingawa dalili zinaonyesha David Moyes ana nia kubwa ya kumfanya Fabregas kuwa Mchezaji wake wa kwanza kumsaini ili aungane na mwenzake aliekuwa nae Arsenal kwa muda mrefu, Robin van Persie.

Wengine wanaotazamwa na Man United kuimarisha Kiungo ni Mchezaji Chipukizi wa Barcelona, Thiago Alcantara na Nahodha wa PSV Kevin Strootman.

Wakati Alcantara ni ‘kinda’, Strootman ni Mchezaji mrefu na mzoefu anaemudu pozisheni zote za Kiungo, iwe Kiungo Mkabaji au Kiungo Mshambuliaji, kitu kinachomfanya awe na uhakika wa kupata namba endapo atatua Old Trafford.

Kiungo gani atatua Old Trafford ndio sakata linalosubiriwa kwa hamu kabla Msimu mpya kuanza hapo Agosti 11 kwa pambano la Fungua Pazia Msimu Mpya la kugombea Ngao ya Jamii kati ya Mabingwa Man United na Mabingwa wa FA CUP Wigan.

No comments:

Post a Comment