SIMBA, MGAMBO SHOOTING ZAINGIZA MIL 16
PATA TAARIFA KAMILI:
Release No. 081
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 10, 2013
KAGERA SUGAR, SHOOTING KUUMANA KAITABA VPL
Kagera Sugar inaikaribisha Ruvu Shooting
ya Pwani katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaofanyika
kesho (Mei 11 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kaitba mjini Bukoba.
Ingawa timu zote mbili hazipambani
kutafuta ubingwa ambao tayari umetwaliwa na Yanga wala kukwepa kushuka
daraja, mechi hiyo bado ni muhimu kwao katika mazingira matatu tofauti.
Kagera Sugar inayonolewa na kocha
mkongwe kuliko wote katika VPL, Abdallah Kibaden na ikiwa na pointi 40
yenyewe inasaka moja kati ya nafasi nne za juu ambazo zina zawadi kutoka
mdhamini wa ligi, lakini pia timu zinazoshika nafasi hizo za juu
zinapata tiketi ya kucheza michuano ya BancABC Super 8.
Kwa upande wa Ruvu Shooting ya Kocha
Charles Boniface Mkwasa yenye pointi 31 inasaka moja ya nafasi sita za
juu ambazo ni fursa ya kuingia kwenye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL
Board) ambayo inatarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika Septemba 28 mwaka huu.
Wagombea nafasi za uenyekiti na makamu
wake ni lazima watoke katika timu zilizoshika nafasi sita la juu katika
VPL msimu uliopita. Uchaguzi wa TPL Board utafanyika siku moja kabla ya
ule wa TFF uliopangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.
Raundi ya 25 ya ligi hiyo itakamilika
keshokutwa (Mei 12 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Mgambo
Shooting ya Tanga. Mechi hiyo namba 169 itachezwa katika Uwanja wa Azam
Complex ulioko Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Azam yenye pointi 48 inahitaji moja
zaidi ili kutetea nafasi yake ya umakamu bingwa iliyoutwaa msimu wa
2011/2013 na kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya
Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Wakati Azam ikisaka pointi hiyo moja,
Mgambo Shooting inayofundishwa na wachezaji wa zamani wa mabingwa wa
Tanzania Bara mwaka 1988, Mohamed Kampira akisaidiwa na Joseph Lazaro ni
moja ya timu ziko katika hatari ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
msimu ujao.
Mgambo Shooting inahitaji pointi moja tu
katika mechi mbili ilizobakiza kukwepa kurudi FDL, ikishindwa kupata
pointi hiyo huku Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza zikishinda
mechi zao za mwisho kwa uwiano mzuri wa mabao itakuwa imekwenda na maji.
Mechi ya Azam dhidi ya Mgambo Shooting
itachezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, na atasaidiwa na Abdallah
Rashid wa Pwani na Charles Mbilinyi wa Mwanza. Mwamuzi wa mezani
atakuwa Idd Lila wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Omari Walii wa
Arusha.
SIMBA, MGAMBO SHOOTING ZAINGIZA MIL 16
Mechi namba 149 ya Ligi Kuu ya Vodacom
kati ya Simba na Mgambo Shooting iliyochezwa juzi (Mei 8 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kushinda
bao 1-0 imeingiza sh. 16,651,000.
Watazamaji 3,006 walikata tiketi
kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000,
sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,226,125
wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,539,983.05.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 1,640,402.54, tiketi sh. 3,175,000, gharama za
mechi sh. 984,241.53, Kamati ya Ligi sh. 984,241.53, Mfuko wa Maendeleo
ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 492,120.76 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 382,760.60.
TFF YATAKA MAELEZO YA BARUA YA FIFA KWA DAUDA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtaka Shaffih Dauda ambaye ni mmiliki wa tovuti ya www.shaffihdauda.com kutoa maelezo kuhusiana na barua ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) aliyoiweka kwenye mtandao wake huo.
FIFA ambayo ilisimamisha mchakato wa
uchaguzi wa TFF baada ya baadhi ya wagombea kuulalamikia, baadaye ilitoa
maelekezo kuhusu mchakato huo kwa barua ambayo iliituma kwa Rais wa
TFF, Leodegar Lenga.
Rais wa TFF katika mkutano wake na
waandishi wa habari ambao Dauda alihudhuria alibainisha kuwa barua hiyo
ya FIFA hawezi kupewa kila mtu, na kuruhusu waandishi kuisoma kwa Ofisa
Habari wa TFF bila kuondoka nayo.
Wakati Rais Tenga anazungumza na
waandishi wa habari (Mei 2 mwaka huu), nakala ya barua hiyo ya FIFA
ilikuwa kwa viongozi wakuu wa TFF pekee, na viongozi wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Hivyo TFF imemtaka Dauda kutoa
maelezo ya mahali alipoipata barua hiyo ndani ya siku saba.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment