Thursday, December 27, 2012

KADI NYEKUNDU GIBSON, COLE ZAFUTWA, FERGIE ANUSURIKA…REDKNAPP, MANCINI….!!!

MANCINI_n_MICAHBosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson hatapata adhabu yeyote toka kwa FA baada ya kumvaa Refa Mike Dean na Wasaidizi wake lakini Mameneja wa Man City, Roberto Mancini, na wa QPR, Harry Redknapp, huenda wakaadhibiwa kwa kauli zao na wakati huo huo Kadi Nyekundu kwa Darron Gibson wa Everton na Carlton Cole wa West Ham zimefutwa.

Chama cha Soka England, FA, kimethibitisha kuwa Sir Alex Ferguson, hatapewa adhabu yeyote kwa kitendo chake cha kabla Kipindi cha Pili kuanza, cha kumvaa Refa Mike Dean na kumlalamikia kisha kumkabili Refa wa Akiba Neil Swarbrick na pia Refa Msaidizi Jake Collin, kwa vile Refa Dean hakuzungumza lolote kuhusu tukio hilo katika Ripoti ya Mechi.

Hata hivyo, Mameneja wa Man City na QPR, Roberto Mancini na Harry Redknapp, wako matatani kufuatia kauli zao baada ya Mechi zao za kulalamika kuhusu Marefa na kudokeza uchezeshaji usio wa haki kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni za FA.

Mancini, Meneja wa Man City, alilalamika kuhusu Refa Kevin Friend baada kufungwa 1-0 na Sunderland kwenye Mechi ya Ligi Kuu England iliyochezwa Desemba 26 kwa Refa huyo kutopiga Filimbi ya Faulo aliyochezewa Mchezaj wake Pablo Zabaleta na badala yake kuachia mpira uchezwe na kuzaa Goli la Adam Johnson, Winga wa zamani wa Man City, lililowaua City 1-0.

Mancini alidai: “Pengine Refa alivimbiwa na Mlo wa Krismasi! Haiwezekani Waamuzi wawili wasione tukio hilo! [Akimaanisha Refa Na Msaidizi wake]”

Nae Harry Redknapp, Bosi wa QPR, yuko matatani baada ya kuhamaki na maamuzi ya Refa Chris Foy ambayo alidai ni ‘Skandali!’ wakati walipofungwa 2-1 na West Brom na kutupwa mkiani mwa Ligi Kuu England Siku ya Boxing Dei.

Refa Chris Foy alilikubali Goli la kujifunga mwenyewe Kipa Robert Green ambae alionekana akibanwa waziwazi na Mchezaji wa WBA, Marc-Antoine Fortune, na pia aliwayima Penati ya wazi mwishoni baada ya Beki Liam Ridgewell kuunawa mpira.

Redknapp amewaka: "Ile ni Faulo ya wazi kwa Kipa wetu na ile ni Penati ya wazi! Hii ni kashfa!”

Msimamo wa FA kwa Mameneja ni kwamba hawatakiwi kuwalaumu Marefa kuhusu maamuzi yao na wakifanya hivyo wanaandikiwa Barua kutaka maelezo yao na kama hayaridhishi hufunguliwa Mashitaka.
Wakati huo huo, FA imetangaza kuwa Rufaa za Everton na West Ham kupinga Kadi Nyekundu kwa Wachezaji wao, Darron Gibson wa Everton na Carlton Cole, zimekubaliwa na Adhabu za kufungiwa Mechi 3 kila mmoja kwa Wachezaji hao zimefutwa.

Wachezaji hao wote wawili walitolewa katika Mechi moja na Refa Mark Anthony Uwanjani Upton Park Wikiendi iliyopita ambako Everton walishinda 2-1 baada ya kutoka nyuma kwa kwa Bao la Carlton Cole na kutolewa kwa Mfungaji huyo kuliwapa mteremko kusawazisha na kushinda huku Mchezaji wao Gibson akitolewa Dakika za majeruhi.

Wachezaji hao wote wawili sasa wako huru kuziwakilisha Klabu zao Mechi za Ligi Wikiendi hii.

No comments:

Post a Comment