Monday, June 3, 2013

RIO FERDINAND: KUFANYIWA MECHI SPESHO KWA UTUMISHI ULIOTUKUKA!

RIO_NA_UBINGWANI OLD TRAFFORD, MAN UNITED v SEVILLA!
MABINGWA Manchester United leo wametangaza kufanyika kwa Mechi maalum ya kutambua Utumishi wa muda mrefu na uliotukuka wa Beki wao Rio Ferdinand.

Mechi hiyo itafanyika Uwanja wa Old Trafford dhidi ya Sevilla ya Spain hapo Agosti 9 ikiwa ni Siku mbili tu kabla ya Man United kucheza Uwanja wa Wembley katika ile Mechi ya kufungua pazia ya Msimu mpya watakapokutana na Wigan Athletics ambao ndio Mabingwa wa FA CUP hapo Agosti 11.

Ferdinand, Miaka 34, Msimu uliokwisha Mwezi Mei alikuwa akitimiza Miaka 11 akiwa na Man United chini ya Meneja aliestaafu hivi karibuni Sir Alex Ferguson na tayari Beki huyo ameongezewa Mwaka mmoja katika Mkataba wake utakaomweka hadi mwisho wa Msimu wa 2013/14.

Mwenyewe Rio Ferdinand amenena: “Hii Klabu ni ya kipekee kwa kila hali, historia yake na msukumo wake huwezi kuamini, unamfanya kila Mtu apiganie kufanikiwa!”

Aliongeza: “Usiku huo utakuwa mkubwa kwangu na utatikisa mawazo yangu! Siamini kama Miaka 10 imepita na nina bahati kuitumikia Man United! Mashabiki wetu ni bora Dunia nzima, wana mapenzi na ninashkuru kwa sapoti yao. Natumai watapata raha Usiku huo!”

Sir Alex Ferguson, ambae alimsaini Ferdinand Mwaka 2002 toka Leeds United, alisema: “Ni kitu muhimu kwa Klabu kuweka Mechi hii spesho kwa Utumishi wake! Yeye ni mmoja wa Mabeki bora Klabu hii imepata kuwa nao! Rio ana kipaji cha asili cha kusoma Mchezo na Mwezi uliokwisha nilitamka kwamba naamini Msimu huu ndio uliokuwa bora katika maisha yake na Man United! Utakuwa Usiku murua kwake na Mashabiki, na pia ni safi kwa kuanza Msimu mpya namna hii!”

Rio Ferdinand ameichezea Man United Mechi 432 na kutwaa Ubingwa wa England mara 6 na Ubingwa wa Ulaya hapo Mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment