MKUTANO MKUU TFF FEBRUARI 23 & 24, 2013
UHAI CUP-NUSU FAINALI KUPIGWA KARUME
TAARIFA KAMILI:
Release No. 199
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 20, 2012
KIM, RENARD KUWAKABILI WAANDISHI KESHO
Makocha wa Tanzania (Taifa Stars), Kim
Poulsen na Zambia (Chipolopolo) watakuwa na mkutano na waandishi wa
habari utakaofanyika kesho (Desemba 21 mwaka huu) kuzungumzia pambano
lao litakalochezwa Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi
kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF). Makocha hao watazungumzia maandalizi yao ya mwisho kabla ya
pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Sylvester Kirwa kuanzia saa 10
kamili jioni.
Pia makocha hao watajibu maswali kutoka
kwa waandishi wa habari kuhusu pambano hilo litakalokutanisha timu hizo
ambazo zimefanya vizuri kwenye orodha ya viwango vya ubora vya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vilivyotolewa jana
(Desemba 19 mwaka huu).
Wakati Zambia ambao ni mabingwa wa
Afrika wamepanda juu kwa viwango vya ubora kwa nafasi nne, Taifa Stars
ambayo katika mchezo uliopita iliifunga Kenya (Harambee Stars) bao 1-0
imepanda kwa nafasi nne.
Taifa Stars ambayo inadhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager iko kambini tangu Desemba 12 mwaka huu
kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya kirafiki inayotarajiwa kuwa ya
kuvutia.
TENGA ATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu
wa Shirikisho hilo tayari ametoa notisi ya mkutano huo utakaofanyika
Februari 23 na 24 mwakani jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo utafanyika Februari 23
mwakani na kufuatiwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata. Ajenda ya
uchaguzi iko chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Notisi hiyo imetumwa kwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu ambao ni kutoka vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama
shiriki, klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na wajumbe wa Kamati ya Utendaji
ya TFF.
Ajenda za Mkutano Mkuu zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya mkutano huo wenye wajumbe zaidi ya 100.
NUSU FAINALI UHAI CUP KUPIGWA KARUME
Mechi za nusu fainali ya michuano ya
Kombe la Uhai 2012 inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya
miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 21
mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo
inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai
itazikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Azam na itafanyika
kuanzia saa 2 kamili asubuhi.
Simba na Coastal Union zitacheza nusu
fainali ya pili kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo.
Mtibwa Sugar imepata tiketi ya nusu fainali baada ya kuichapa African
Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza Oljoro JKT mabao 2-0.
Nayo Azam iliindoa JKT Ruvu kwenye robo
fainali kwa bao 1-0 huku Coastal Union ikipata ushindi wa penalti 4-3
dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya robo fainali.
Mechi ya fainali na ile ya kutafuta
mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mechi ya mshindi wa tatu
itaanza saa 2 kamili asubuhi wakati ya fainali itakuwa saa 10 kamili
jioni.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TWFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba
19 mwaka huu) hoteli ya Midlands mjini Morogoro.
Ushindi aliopata Lina Kessy
aliyechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati
ya Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA
walivyo na imani kwao.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake
kwa Kamati ya Utendaji ya TWFA, na kwamba ina changamoto kubwa ya
kuhakikisha inaendesha shughuli za chama hicho kwa kuzingatia katiba na
kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya
Uchaguzi ya TWFA chini ya Mama Ombeni Zavala na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo
unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia Katiba ya TWFA na Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na
Lina Kessy (Mwenyekiti), Rose Kissiwa (Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma
(Katibu), Zena Chande (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF) wakati mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ni Triphonia Temba.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment