Thursday, December 27, 2012

SIMBA: HUKU ‘GOGORO’ LANUKIA, KOCHA MPYA KUTUA LEO!!

SIMBA-normalWakati Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, akitamka kuwa Mkutano wa Wanachama uliotishwa na Kundi linalodaiwa kuongozwa na Mohamed Wandi si halali, zipo taarifa kuwa Kocha mpya wa Klabu hiyo, Patrick Liewing, kutoka Ufaransa atatua Nchini leo.
Akizungumzia Mkutano huo ulioitishwa na Kundi la Mohamed Wandi ambalo limeripotiwa kukusanya Saini za Wanachama 698 ili kufanya Mkutano wa Wanachama Jumapili hii kwenye Hoteli ya Traventine Jijini Dar es Salaam, Rage amesema uchunguzi wa Watu hao 698 umebaini kuwa 490 kati yao si Wanachama hai kwa vile hawajalipa Ada zao za Uanachama na wengine kati yao ni Marehemu.
Akithibitisha kupokea Barua ya kuitishwa Mkutano huo wa Dharura wa Wanachama, Rage amesema Kikatiba mwenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Dharura wa Wanachama ni Mwenyekiti au Wanachama hai 600.
Kutokana na hitilafu hizo za Kisheria, Rage amesema Uongozi wake hautautambua Mkutano huo.
Pia, Rage amedai Kundi la Viongozi wa zamani ndio wanaotaka kuitisha Mkutano huo kinyume cha Katiba yao.
Hata hivyo, Mohamed Wandi amekaririwa akitamka kuwa Mkutano huo hauna nia mbaya ila tu ni kuchambua mwendo mbovu wa Simba katika mzunguko wa Kwanza wa Ligi Kuu Vodacom ambao walianza vizuri mno lakini wakamaliza vibaya na kutupwa nafasi ya 3 huku juu yao wapo Azam FC na vinara ni Mahasimu wao wakubwa, Yanga.
Wakati huo huo, Ismail Aden Rage, amethibitisha ujio wa Kocha wao mpya, Patrick Liewing, kutoka Ufaransa ambae atatua Nchini leo.
Rage amesema Kocha huyo, ambae aliwahi kufundisha Timu za Vijana za Klabu maarufu huko France, Paris Saint Germain, atakuwa Kocha Mkuu na pia atapewa jukumu la kuendeleza vipaji vya Vijana.
Rage amesema: “Simba ndio Timu pekee Nchini yenye mfumo wa kuendeleza Vijana na zipo timu za Vijana chini ya Miaka 14, 16 17 na 20! Ujio wa Liewing utatusaidia sana kwa sababu ana uzoefu wa kukuza vipaji!”
Kocha huyo mpya kesho anatarajiwa kukutana na Wachezaji wote kwenye Kambi yao ya Mazoezi huko TCC Chang’ombe, Dar es Salaam.
Liewing, ambae anambadili Kocha kutoka Serbia Milovan Cirkovic, aliwahi kuwa Kocha wa Asec Mimosa ya Ivory Coast kati ya Mwaka 2004 na 2009 na kuisaidia kutwaa Makombe kadhaa Nchini humo pamoja na kuifikisha Nusu Fainali ya CAF CHAMPIONZ LIGI Mwaka 2009.
Mwaka 2006, Kocha Liewing pamoja na Kocha wa Al Ahly ya Misri waliteuliwa kuwa Makocha Bora Afrika.

No comments:

Post a Comment